MEGA.Bible Tafuta
Kiswahili

The Parable of the Sower

Biblia Takatifu (Swahili)

Mat 13:1–9

  1. 1 Siku hiyo hiyo Isa akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari.
  2. 2 Umati mkubwa mno wa watu wakakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari.
  3. 3 Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake.
  4. 4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.
  5. 5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba.
  6. 6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.
  7. 7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea.
  8. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini.
  9. 9 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

Mrk 4:1–9

  1. 1 Isa akaanza kufundisha tena kando ya bahari. Palikuwa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika kumzunguka, hata ikambidi Isa aingie kwenye mashua iliyokuwa baharini na kuketi humo, nao watu wote walikuwa ufuoni mwa bahari.
  2. 2 Akawafundisha mambo mengi kwa mifano, naye katika mafundisho yake akasema:
  3. 3 “Sikilizeni! Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu
  4. 4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila.
  5. 5 Nyingine zilianguka kwenye mwamba usio na udongo mwingi. Ziliota haraka kwa kuwa udongo ulikuwa kidogo.
  6. 6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina.
  7. 7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba ikakua, ikaisonga hiyo mimea, hivyo haikutoa mazao.
  8. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri, zikaota vizuri na kukua, zikatoa mazao, moja mara thelathini, nyingine mara sitini, na nyingine mara mia moja.”
  9. 9 Kisha Isa akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

Luk 8:4–8

  1. 4 Umati mkubwa wa watu walipokuwa wakikusanyika, nao watu walikuwa wakimjia Isa kutoka kila mji, akawaambia mfano huu:
  2. 5 “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia; zikakanyagwa, nao ndege wa angani wakazila.
  3. 6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu.
  4. 7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo ile miiba ikakua pamoja nazo, na kuisonga hiyo mimea.
  5. 8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia moja zaidi ya mbegu alizopanda.” Baada ya kusema haya, Isa akapaza sauti, akasema, “Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”