Zaburi 121
1 Nayainua macho yangu natazama milima: msaada wangu utatoka wapi?
2 Msaada wangu hutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia.
3 Hatauacha mguu wako uteleze, yeye akulindaye hatasinzia,
4 hakika, yeye alindaye Israeli hatasinzia wala hatalala usingizi.
5 Mwenyezi Mungu anakulinda, Mwenyezi Mungu ni uvuli wako mkono wako wa kuume,
6 jua halitakudhuru mchana, wala mwezi wakati wa usiku.
7 Mwenyezi Mungu atakukinga na madhara yote, atayalinda maisha yako,
8 Mwenyezi Mungu atakulinda unapoingia na unapotoka, tangu sasa na hata milele.