Waisraeli wote, wakiwa na wazee wao, maafisa na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu, wakiwaelekea makuhani Walawi waliokuwa wamelibeba. Wageni walioishi miongoni mwao, pamoja na wazawa, walikuwa hapo. Nusu ya watu walisimama mbele ya Mlima Gerizimu, na nusu nyingine wakasimama mbele ya Mlima Ebali, kama vile Musa mtumishi wa Mwenyezi Mungu alivyokuwa ameamuru hapo mwanzo alipotoa maagizo ya kuwabariki watu wa Israeli.