The Fall of Jerusalem
Biblia Takatifu (Swahili)
2Ki 25:1–21
- 1 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli, akiwa na jeshi lake lote, alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Akapiga kambi nje ya mji na kuuzingira pande zote.
- 2 Mji ulizingirwa na jeshi hadi mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.
- 3 Ilipofika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.
- 4 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa, na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba.
- 5 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia mfalme na kumpata katika nchi tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika,
- 6 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, ambapo hukumu yake ilitangazwa.
- 7 Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Kisha wakayang’oa macho yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli.
- 8 Siku ya saba ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme, afisa wa mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu.
- 9 Alichoma moto Hekalu la Mwenyezi Mungu, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu.
- 10 Jeshi lote la Wakaldayo, chini ya mkuu wa askari walinzi wa mfalme, walivunja kuta zilizoizunguka Yerusalemu.
- 11 Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi akawapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli.
- 12 Lakini yule jemadari wa askari walinzi akawaacha baadhi ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
- 13 Wakaldayo walivunja vipande vipande zile nguzo za shaba, vile vishikilio vya shaba vilivyohamishika, na ile Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hivyo wakaichukua hiyo shaba na kuipeleka Babeli.
- 14 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika katika huduma ya Hekalu.
- 15 Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua vile vyetezo na yale mabakuli ya kunyunyizia, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
- 16 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika.
- 17 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane. Sehemu ya shaba juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tatu na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na wavu wake ilifanana na hiyo ya kwanza.
- 18 Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu.
- 19 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua kiongozi wa wapiganaji, na washauri watano wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji.
- 20 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.
- 21 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani mbali na nchi yao.
2Ch 36:17–21
- 17 Mungu akamwinua dhidi yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao wa kiume kwa upanga ndani ya mahali patakatifu. Hakumbakiza kijana wala mwanamwali, mzee wala mnyonge. Mungu akawatia wote mikononi mwa Nebukadneza.
- 18 Akavichukua kwenda Babeli vyombo vyote kutoka Hekalu la Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za Hekalu la Mwenyezi Mungu pamoja na hazina za mfalme na za maafisa wake.
- 19 Wakalichoma Hekalu la Mungu na kuzibomoa kuta za Yerusalemu, wakachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu kila kitu chake cha thamani.
- 20 Wale watu walionusurika kuuawa kwa upanga wakachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Nao wakawa watumishi wake na wa wanawe hadi wakati wa utawala wa ufalme wa Uajemi ulifika.
- 21 Nchi ikaendelea kufurahia pumziko zake za sabato; wakati wote wa kufanywa kwake ukiwa ilipumzika, hadi ile miaka sabini ilipotimia katika kutimiza neno la Mwenyezi Mungu lililonenwa na Yeremia.
Jer 52:4–27
- 4 Hivyo katika mwaka wa tisa wa utawala wa Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli akiwa na jeshi lake lote alifanya vita dhidi ya Yerusalemu. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzingira pande zote.
- 5 Mji ulizingirwa na jeshi hadi mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Mfalme Sedekia.
- 6 Ilipowadia siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ikazidi kuwa kali sana ndani ya mji, hadi hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.
- 7 Kisha ukuta wa mji ukavunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia lango lililokuwa kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Wakakimbia kuelekea Araba.
- 8 Lakini jeshi la Wakaldayo likamfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika nchi tambarare za Yeriko. Askari wake wote wakatengwa naye na kutawanyika,
- 9 naye akakamatwa. Akapelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ambapo alimtangazia hukumu.
- 10 Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake. Pia akawaua maafisa wote wa Yuda.
- 11 Kisha akayang’oa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli, alipomweka gerezani hadi siku ya kifo chake.
- 12 Siku ya kumi ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme, aliyemtumikia mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu.
- 13 Alichoma moto Hekalu la Mwenyezi Mungu, jumba la kifalme, na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu.
- 14 Jeshi lote la Wakaldayo chini ya mkuu wa askari walinzi wa mfalme walivunja kuta zote zilizoizunguka Yerusalemu.
- 15 Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, akawapeleka uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa kawaida, na wale waliojisalimisha kwa mfalme wa Babeli.
- 16 Lakini Nebuzaradani akawaacha mabaki ya wale watu maskini kabisa ili watunze mashamba ya mizabibu na mashamba mengine.
- 17 Wakaldayo walivunja nguzo za shaba, vishikilio vya shaba, na Bahari ya shaba, ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Kisha wakaichukua shaba yote wakaipeleka Babeli.
- 18 Wakachukua pia vyungu, masepetu, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, sahani na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika Hekaluni.
- 19 Mkuu wa askari walinzi wa mfalme akachukua yale masinia, vile vyetezo, yale mabakuli ya kunyunyizia, zile sufuria, vile vinara vya taa, zile sahani na yale mabakuli yaliyotumika kwa sadaka za vinywaji, vitu vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.
- 20 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na wale mafahali kumi na wawili wa shaba waliokuwa chini yake, pamoja na vile vishikilio vilivyohamishika, ambavyo Mfalme Sulemani alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, ilikuwa na uzito mwingi usioweza kupimika.
- 21 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kimo chake na mzunguko dhiraa kumi na mbili, na unene wa nyanda nne, na zote zilikuwa wazi ndani.
- 22 Sehemu ya shaba juu ya ile nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tano, na ilikuwa imepambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Ile nguzo nyingine pamoja na makomamanga yake ilifanana na hiyo ya kwanza.
- 23 Kulikuwa na makomamanga tisini na sita pembeni; jumla ya makomamanga juu ya wavu uliokuwa umezunguka yalikuwa mia moja.
- 24 Yule mkuu wa askari walinzi akawachukua kama wafungwa Seraya kuhani mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo, na mabawabu watatu.
- 25 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji, na washauri saba wa mfalme. Akamchukua pia mwandishi aliyesimamia uandikishaji wa watu wa nchi, pamoja na watu wake sitini waliopatikana ndani ya mji.
- 26 Nebuzaradani jemadari akawachukua hao wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.
- 27 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme wa Babeli akaamuru wanyongwe. Hivyo Yuda wakaenda utumwani, mbali na nchi yao.