The Death of John the Baptist
Biblia Takatifu (Swahili)
Mat 14:1–12
- 1 Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Isa,
- 2 akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yahya; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
- 3 Herode alikuwa amemkamata Yahya, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake,
- 4 kwa kuwa Yahya alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.”
- 5 Herode alitaka sana kumuua Yahya, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.
- 6 Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana,
- 7 kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba.
- 8 Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yahya kwenye sinia.”
- 9 Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake.
- 10 Hivyo akaagiza Yahya akatwe kichwa mle gerezani.
- 11 Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake.
- 12 Wanafunzi wa Yahya wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Isa.
Mrk 6:14–29
- 14 Mfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Isa lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”
- 15 Wengine wakasema, “Yeye ni Ilya.” Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmoja wa manabii wa zamani.”
- 16 Lakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yahya, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”
- 17 Herode mwenyewe alikuwa ameagiza kwamba Yahya akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa.
- 18 Yahya alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.”
- 19 Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yahya kinyongo, akataka kumuua. Lakini hakuweza,
- 20 kwa sababu Herode alimwogopa Yahya akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yohana, lakini bado alipenda kumsikiliza.
- 21 Hatimaye Herodia alipata wakati mwafaka aliokuwa akiutafuta. Mfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya.
- 22 Binti Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani. Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.”
- 23 Tena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”
- 24 Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?” Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yahya.”
- 25 Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yahya kwenye sinia.”
- 26 Mfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia.
- 27 Mara mfalme akatuma askari mmoja wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yahya. Akaenda na kumkata Yahya kichwa humo gerezani,
- 28 akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake.
- 29 Wanafunzi wa Yahya walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Luk 9:7–9
- 7 Basi Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za yote yaliyotendeka. Naye akafadhaika, kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yahya amefufuliwa kutoka kwa wafu.
- 8 Wengine wakasema Ilya amewatokea, na wengine kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka.
- 9 Herode akasema, “Yahya nilimkata kichwa. Lakini ni nani huyu ninayesikia mambo kama haya kumhusu?” Akatamani sana kumwona.