MEGA.Bible Tafuta
Kiswahili

The Death of Jesus

Biblia Takatifu (Swahili)

Mat 27:45–56

  1. 45 Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote.
  2. 46 Ilipofika saa tisa, Isa akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
  3. 47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Ilya.”
  4. 48 Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe.
  5. 49 Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumwokoa.”
  6. 50 Isa alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.
  7. 51 Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka.
  8. 52 Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa.
  9. 53 Wakatoka makaburini, na baada ya Isa kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.
  10. 54 Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Isa walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa sana, wakapaza sauti na kusema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
  11. 55 Wanawake wengi walikuwa pale wakitazama kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Isa tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake.
  12. 56 Miongoni mwao walikuwemo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Mrk 15:33–41

  1. 33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa.
  2. 34 Hapo saa tisa, Isa akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
  3. 35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Ilya.”
  4. 36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”
  5. 37 Kisha Isa akatoa sauti kuu, akakata roho.
  6. 38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini.
  7. 39 Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Isa aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
  8. 40 Palikuwa na wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwa Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome.
  9. 41 Hawa walifuatana na Isa na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwako wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye hadi Yerusalemu.

Luk 23:44–49

  1. 44 Ilikuwa kama saa sita mchana, nalo giza likafunika nchi yote hadi saa tisa,
  2. 45 kwa sababu jua liliacha kutoa nuru. Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili.
  3. 46 Isa akapaza sauti yake akasema, “Baba, mikononi mwako naikabidhi roho yangu.” Baada ya kusema haya, akakata roho.
  4. 47 Yule jemadari alipoona yaliyotukia, akamsifu Mungu, akasema, “Hakika, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”
  5. 48 Watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo kushuhudia tukio hili walipoyaona hayo, wakapigapiga vifua vyao kwa huzuni na kwenda zao.
  6. 49 Lakini wale wote waliomfahamu, pamoja na wale wanawake waliokuwa wamemfuata kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiyatazama mambo haya.

Jhn 19:28–30

  1. 28 Baada ya haya, akijua kuwa mambo yote yamemalizika, na ili kutimiza Maandiko, Isa akasema, “Naona kiu.”
  2. 29 Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni.
  3. 30 Baada ya kuionja hiyo siki, Isa akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.