The Call of Matthew (Levi)
Biblia Takatifu (Swahili)
Mat 9:9–13
- 9 Isa alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akasimama, akamfuata.
- 10 Isa alipokuwa ameketi akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na wenye dhambi wakaja, wakaketi kula pamoja naye na wanafunzi wake.
- 11 Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”
- 12 Lakini Isa aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu.
- 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Mrk 2:13–17
- 13 Isa akaenda tena kandokando ya Bahari ya Galilaya. Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akaanza kuwafundisha.
- 14 Alipokuwa akitembea, akamwona Lawi mwana wa Alfayo ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Naye Lawi akaondoka, akamfuata Isa.
- 15 Isa alipokuwa ameketi akila chakula nyumbani mwa Lawi, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wakila pamoja naye na wanafunzi wake, kwa maana ni watu wengi waliokuwa wakimfuata.
- 16 Walimu wa Torati waliokuwa Mafarisayo walipomwona akila pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, wakawauliza wanafunzi wake: “Mbona Isa anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”
- 17 Isa aliposikia haya akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Luk 5:27–32
- 27 Baada ya haya, Isa alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kutoza ushuru. Akamwambia, “Nifuate.”
- 28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.
- 29 Kisha Lawi akamfanyia Isa karamu kubwa nyumbani mwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao.
- 30 Lakini Mafarisayo na walimu wa Torati waliokuwa wa dhehebu lao wakawalalamikia wanafunzi wa Isa, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”
- 31 Isa akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa.
- 32 Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”