The Arrest of Jesus
Biblia Takatifu (Swahili)
Mat 26:47–56
- 47 Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.
- 48 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.”
- 49 Mara Yuda akamjia Isa na kumsalimu, “Salamu, Mwalimu!” Akambusu.
- 50 Isa akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.” Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Isa.
- 51 Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Isa alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
- 52 Ndipo Isa akamwambia, “Rudisha upanga wako alani mwake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga.
- 53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?
- 54 Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
- 55 Wakati huo, Isa akaambia wale umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata?
- 56 Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Mrk 14:43–52
- 43 Isa alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa Torati, na wazee.
- 44 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.”
- 45 Mara Yuda akamjia Isa na kusema, “Mwalimu.” Akambusu.
- 46 Wale watu wakamkamata Isa, wakamweka chini ya ulinzi.
- 47 Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
- 48 Kisha Isa akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyang’anyi?
- 49 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.”
- 50 Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
- 51 Kijana mmoja, aliyekuwa amevaa nguo ya kitani pekee, alikuwa akimfuata Isa. Walipomkamata,
- 52 alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
Luk 22:47–53
- 47 Isa alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu wakaja. Waliongozwa na Yuda, aliyekuwa mmoja wa wale kumi na wawili. Akamkaribia Isa ili ambusu.
- 48 Lakini Isa akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
- 49 Wafuasi wa Isa walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?”
- 50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
- 51 Lakini Isa akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
- 52 Kisha Isa akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyang’anyi?
- 53 Kila siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
Jhn 18:1–11
- 1 Isa alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake, wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani; yeye na wanafunzi wake wakaingia humo.
- 2 Basi Yuda, aliyemsaliti, alipafahamu mahali hapo, kwani Isa alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara.
- 3 Hivyo Yuda akaja kwenye bustani akiongoza kikosi cha askari Warumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha.
- 4 Isa, akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao, akawauliza, “Mnamtafuta nani?”
- 5 Wao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.” Isa akawajibu, “Mimi ndiye.” (Yuda, aliyemsaliti, alikuwa amesimama pamoja nao.)
- 6 Isa alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!
- 7 Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?” Nao wakamjibu, “Isa Al-Nasiri.”
- 8 Isa akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.”
- 9 Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”
- 10 Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. (Mtumishi huyo aliitwa Malko.)
- 11 Isa akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?”