MEGA.Bible Tafuta
Kiswahili

Signs of the End of the Age

Biblia Takatifu (Swahili)

Mat 24:1–8

  1. 1 Isa akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonesha majengo ya Hekalu.
  2. 2 Ndipo Isa akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
  3. 3 Isa alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”
  4. 4 Isa akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye.
  5. 5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Al-Masihi,’ nao watawadanganya wengi.
  6. 6 Mtasikia habari za vita na tetesi za vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado.
  7. 7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.
  8. 8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu.

Mrk 13:1–8

  1. 1 Isa alipokuwa akitoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu! Tazama jinsi mawe haya yalivyo makubwa, na majengo haya yalivyo mazuri!”
  2. 2 Ndipo Isa akajibu akasema, “Je, unayaona majengo haya yalivyo makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali yote yatabomolewa.”
  3. 3 Isa alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni mkabala na Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea wakamuuliza faraghani,
  4. 4 “Tafadhali tuambie, mambo haya yatatukia lini? Nayo dalili ya kuwa hayo yote yanakaribia kutimia itakuwa gani?”
  5. 5 Isa akawaambia: “Jihadharini mtu yeyote asiwadanganye.
  6. 6 Wengi watakuja kwa Jina langu wakidai, ‘Mimi ndiye,’ nao watawadanganya wengi.
  7. 7 Msikiapo habari za vita na uvumi wa vita, msiwe na hofu. Mambo haya hayana budi kutukia, lakini ule mwisho bado.
  8. 8 Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali na njaa. Haya yatakuwa ndio mwanzo wa uchungu.

Luk 21:5–11

  1. 5 Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Isa akawaambia,
  2. 6 “Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
  3. 7 Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonesha kwamba yanakaribia kutendeka?”
  4. 8 Isa akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate.
  5. 9 Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”
  6. 10 Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine.
  7. 11 Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.