MEGA.Bible Tafuta
Kiswahili

Plucking Grain on the Sabbath

Biblia Takatifu (Swahili)

Mat 12:1–8

  1. 1 Wakati huo Isa alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala.
  2. 2 Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”
  3. 3 Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa?
  4. 4 Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani tu.
  5. 5 Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia?
  6. 6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa.
  7. 7 Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia,
  8. 8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Mrk 2:23–28

  1. 23 Siku moja ya Sabato, Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wakipita katikati ya mashamba ya nafaka. Walipokuwa wakitembea, wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke.
  2. 24 Mafarisayo wakamwambia, “Tazama, mbona wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato?”
  3. 25 Isa akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi yeye na wenzake walipokuwa na njaa, wakahitaji chakula?
  4. 26 Daudi aliingia katika nyumba ya Mungu, Abiathari alipokuwa kuhani mkuu, akaila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.”
  5. 27 Kisha Isa akawaambia, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, lakini si mwanadamu kwa ajili ya Sabato.
  6. 28 Hivyo, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Luk 6:1–5

  1. 1 Ikawa siku moja ya Sabato Isa alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, nao wanafunzi wake wakaanza kuvunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake.
  2. 2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo yasiyo halali kufanywa siku ya Sabato?”
  3. 3 Isa akawajibu, “Je, ninyi hamjasoma alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walikuwa na njaa?
  4. 4 Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua na kuila ile mikate iliyowekwa wakfu, ambayo ni halali kuliwa na makuhani tu. Naye pia akawapa wenzake.”
  5. 5 Kisha Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”