Zaburi 141
1 Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita, njoo kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita.
2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.
3 Ee Mwenyezi Mungu, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda maovu.
6 Watawala wao watatupwa chini kutoka majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli.
7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”
8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.
9 Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda maovu.
10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama.