Zaburi 12

1 Mwenyezi Mungu tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.

2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.

3 Mwenyezi Mungu na akatilie mbali midomo yote ya hila na kila ulimi uliojaa majivuno,

4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”

5 “Kwa sababu wanyonge wanaonewa, na wahitaji wanalia kwa uchungu, nitainuka sasa,” asema Mwenyezi Mungu. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.”

6 Maneno ya Mwenyezi Mungu ni safi, kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, iliyosafishwa mara saba.

7 Ee Mwenyezi Mungu, utatuweka salama na kutulinda na kizazi hiki milele.

8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali wakati yule aliye mbaya sana ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.