The Burial of Jesus
Biblia Takatifu (Swahili)
Mat 27:57–61
- 57 Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yusufu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Isa.
- 58 Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Isa. Pilato akaamuru apewe.
- 59 Yusufu akauchukua mwili wa Isa, akaufunga kwa kitambaa cha kitani safi,
- 60 na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake.
- 61 Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walikuwa mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.
Mrk 15:42–47
- 42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi (yaani siku moja kabla ya Sabato),
- 43 Yusufu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na alikuwa anautarajia ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Isa.
- 44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Isa alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Isa alikuwa amekwisha kufa.
- 45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yusufu ruhusa ya kuuchukua huo mwili.
- 46 Hivyo Yusufu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi.
- 47 Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.
Luk 23:50–56
- 50 Basi kulikuwa na mtu mmoja mwema na mwenye haki, jina lake Yusufu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza la Wayahudi,
- 51 lakini yeye hakuwa amekubaliana na maamuzi na vitendo vya viongozi wenzake. Huyu alikuwa raia wa Arimathaya huko Yudea, naye alikuwa anaungojea ufalme wa Mungu kwa matarajio makubwa.
- 52 Yusufu alienda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Isa.
- 53 Akaushusha kutoka msalabani, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, na kuuweka katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limezikiwa mtu mwingine bado.
- 54 Ilikuwa Siku ya Maandalizi, nayo Sabato ilikuwa karibu kuanza.
- 55 Wale wanawake waliokuwa wamekuja pamoja na Isa wakimfuata kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Isa ulivyolazwa.
- 56 Kisha wakarudi nyumbani, wakaandaa manukato na marhamu ya kuupaka huo mwili. Lakini wakapumzika siku ya Sabato kama ilivyoamriwa.
Jhn 19:38–42
- 38 Baada ya mambo haya, Yusufu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Isa, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Isa. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua.
- 39 Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Isa usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini.
- 40 Wakauchukua mwili wa Isa, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi.
- 41 Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado.
- 42 Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Isa humo.