Josiah and the Book of the Law
Biblia Takatifu (Swahili)
2Ki 22:1–20
- 1 Yosia alikuwa na umri wa miaka nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na moja. Mama yake aliitwa Yedida binti Adaya, kutoka Boskathi.
- 2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia zote za Daudi baba yake. Hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
- 3 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akasema:
- 4 “Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu.
- 5 Waambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu:
- 6 wale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu.
- 7 Lakini hawahitajiki kutoa maelezo ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kazi kwa uaminifu.”
- 8 Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma.
- 9 Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.”
- 10 Ndipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari, akisema: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme.
- 11 Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Torati, akararua mavazi yake.
- 12 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme:
- 13 “Nendeni mkamuulize Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Mwenyezi Mungu ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu.”
- 14 Hilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili.
- 15 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu,
- 16 ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma.
- 17 Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’
- 18 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Mwenyezi Mungu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia:
- 19 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Mwenyezi Mungu.
- 20 Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ” Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.
2Ch 34:8–28
- 8 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yosia, ili kutakasa nchi na Hekalu, akawatuma Shafani, mwana wa Azalia na Maaseya mtawala wa mji, pamoja na Yoa mwana wa Yoahazi, mwandishi ili kukarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
- 9 Wakamwendea Hilkia kuhani mkuu na kumpa fedha ambazo zilikuwa zimeletwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu ambazo Walawi waliokuwa mabawabu walikuwa wamezikusanya kutoka kwa watu wa Manase, Efraimu na mabaki wote wa Israeli kutoka kwa watu wote wa Yuda na Benyamini na wakazi wa Yerusalemu.
- 10 Kisha wakazikabidhi hizo fedha kwa watu waliowekwa ili kusimamia kazi ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. Hawa watu waliwalipa wafanyakazi waliokarabati na kutengeneza Hekalu lipate kurudi katika hali yake.
- 11 Wakawapa pia mafundi seremala na waashi fedha ili kununua mawe yaliyochongwa, mbao kwa ajili ya kufungia na boriti kwa ajili ya majengo ambayo wafalme wa Yuda walikuwa wameyaacha yakawa magofu.
- 12 Watu wakafanya kazi kwa uaminifu. Waliokuwa wamewekwa juu yao ili kuwaelekeza ni Yahathi na Obadia, Walawi wa uzao wa Merari, Zekaria na Meshulamu, waliotoka kwenye uzao wa Kohathi. Walawi wote wenye ujuzi wa kupiga ala za uimbaji,
- 13 wakawa wasimamizi wa vibarua na kuwaongoza wale waliofanya kila aina ya kazi. Baadhi ya Walawi walikuwa waandishi, maafisa na mabawabu.
- 14 Wakati walikuwa wakizitoa nje fedha zilizokuwa zimetolewa kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu, kuhani Hilkia akakipata kile Kitabu cha Torati ya Mwenyezi Mungu kilichokuwa kimetolewa kwa mkono wa Musa.
- 15 Hilkia akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” Akampa Shafani kile Kitabu.
- 16 Kisha Shafani akakipeleka kile Kitabu kwa mfalme na kumwambia, “Maafisa wako wanafanya kila kitu kama walivyokabidhiwa kufanya.
- 17 Wamelipa fedha zilizokuwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu na wamewakabidhi wasimamizi na wafanyakazi.”
- 18 Kisha Shafani mwandishi akamwarifu mfalme kuwa, “Kuhani Hilkia amenipa Kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
- 19 Mfalme aliposikia yale maneno ya Torati, akayararua mavazi yake.
- 20 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani, Abdoni mwana wa Mika, Shafani mwandishi na Asaya mtumishi wa mfalme,
- 21 “Nendeni mkamuulize Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu na kwa ajili ya mabaki waliosalia katika Israeli na Yuda, kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Mwenyezi Mungu iliyomwagwa juu yetu ni kubwa mno kwa sababu baba zetu hawakulishika neno la Mwenyezi Mungu wala hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa katika Kitabu hiki.”
- 22 Hilkia pamoja na wale wote mfalme aliokuwa amewatuma pamoja naye wakaenda kuzungumza na nabii mke aitwaye Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tokhathi, mwana wa Hasra mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu, katika Mtaa wa Pili.
- 23 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu,
- 24 ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Nitaleta maafa mahali hapa na kwa watu wake: laana zote zilizoandikwa ndani ya kitabu hicho, ambazo zimesomwa mbele ya mfalme wa Yuda.
- 25 Kwa sababu wameniacha na kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kunighadhibisha kwa kazi yote ya mikono yao, hivyo hasira yangu itamwagwa mahali hapa, wala haitatulizwa.’
- 26 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Mwenyezi Mungu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia:
- 27 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake na kwa sababu ulijinyenyekeza mbele zangu na uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Mwenyezi Mungu.
- 28 Basi nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa na juu ya wote wanaoishi hapa.’ ” Kwa hiyo wakampelekea mfalme jibu lake.