MEGA.Bible Tafuta
Kiswahili

Healing the Epileptic Boy

Biblia Takatifu (Swahili)

Mat 17:14–21

  1. 14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Isa na kupiga magoti mbele yake, akasema,
  2. 15 “Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji.
  3. 16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”
  4. 17 Isa akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.”
  5. 18 Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona tangu saa hiyo.
  6. 19 Kisha wanafunzi wakamwendea Isa wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
  7. 20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [
  8. 21 Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”

Mrk 9:14–29

  1. 14 Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa Torati wakibishana nao.
  2. 15 Mara wale watu walipomwona Isa, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.
  3. 16 Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”
  4. 17 Mtu mmoja miongoni mwa umati ule wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea.
  5. 18 Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
  6. 19 Isa akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini! Nitakuwa pamoja nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana kwangu.”
  7. 20 Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Isa, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
  8. 21 Isa akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake.
  9. 22 Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”
  10. 23 Isa akamwambia, “Ati, ‘Kama unaweza kufanya jambo lolote’? Yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”
  11. 24 Mara baba yake yule mvulana akapaza sauti akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!”
  12. 25 Isa alipoona kwamba umati wa watu wanakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”
  13. 26 Baada ya yule pepo mchafu kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.”
  14. 27 Lakini Isa akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
  15. 28 Baada ya Isa kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”
  16. 29 Isa akawajibu, “Pepo aina hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba [na kufunga].”

Luk 9:37–43

  1. 37 Kesho yake waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu.
  2. 38 Mtu mmoja katika umati ule akapaza sauti, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, kwani ndiye mtoto wangu wa pekee.
  3. 39 Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige mayowe, kisha humwangusha na kumtia kifafa hata akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana, na hamwachi ila mara chache.
  4. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
  5. 41 Isa akawajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia hadi lini? Mlete mwanao hapa.”
  6. 42 Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Isa akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, na akamrudisha kwa baba yake.
  7. 43 Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu walikuwa wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Isa, yeye akawaambia wanafunzi wake: