Zaburi 16

1 Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia.

2 Nilimwambia Mwenyezi Mungu, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema.”

3 Kuhusu watakatifu walio duniani, hao ndio wenye fahari, na ninapendezwa nao.

4 Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo, au kutaja majina yao mdomoni mwangu.

5 Mwenyezi Mungu umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.

6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri.

7 Nitamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.

8 Nimemweka Mwenyezi Mungu mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika.

9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama,

10 kwa maana hutaniacha Kuzimu, wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu.

11 Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha ya milele katika mkono wako wa kuume.