Zaburi 127
1 Mwenyezi Mungu asipoijenga nyumba, wajengao hufanya kazi bure. Mwenyezi Mungu asipoulinda mji, walinzi wakesha bure.
2 Mnajisumbua bure kuamka mapema na kuchelewa kulala, mkitaabikia chakula: kwa maana yeye huwapa usingizi wapendwa wake.
3 Watoto ni urithi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, uzao ni zawadi kutoka kwake.
4 Kama mishale mikononi mwa shujaa ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake.
5 Heri mtu ambaye podo lake limejazwa nao. Hawataaibishwa wanaposhindana na adui zao langoni.