Zaburi 125

1 Wale wamtumainio Mwenyezi Mungu ni kama Mlima Sayuni, ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele.

2 Kama milima inavyozunguka Yerusalemu, ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowazunguka watu wake sasa na hata milele.

3 Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi waliyopewa wenye haki, ili wenye haki wasije wakatumia mikono yao kutenda ubaya.

4 Ee Mwenyezi Mungu, watendee mema walio wema, wale walio wanyofu wa moyo.

5 Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka, Mwenyezi Mungu atawafukuza pamoja na watenda maovu. Amani iwe juu ya Israeli.