Zaburi 112

1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Heri mtu yule amchaye Mwenyezi Mungu, mtu yule apendezwaye sana na amri zake.

2 Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi, kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa.

3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri, haki yake hudumu milele.

4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu, yule mwenye rehema, huruma na haki.

5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba, anayefanya mambo yake kwa haki.

6 Hakika hatatikisika kamwe, mtu mwenye haki atakumbukwa milele.

7 Hataogopa habari mbaya, moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Mwenyezi Mungu.

8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu, mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake.

9 Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele; pembe yake itatukuzwa kwa heshima.

10 Mtu mwovu ataona na kuchukizwa, atasaga meno yake na kutoweka, kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.