Zaburi 124

1 Kama Mwenyezi Mungu hangekuwa upande wetu; Israeli na aseme sasa:

2 kama Mwenyezi Mungu hangekuwa upande wetu, watu walipotushambulia,

3 hasira yao ilipowaka dhidi yetu, wangetumeza tukiwa hai,

4 mafuriko yangegharikisha, maji mengi yangetufunika,

5 maji yaendayo kasi yangetuchukua.

6 Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.

7 Tumeponyoka kama ndege kutoka mtego wa mwindaji; mtego umevunjika, nasi tumeokoka.

8 Msaada wetu ni katika jina la Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na dunia.