Zaburi 96

1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya; mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote.

2 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, lisifuni jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.

3 Tangazeni utukufu wake katika mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.

4 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.

5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu.

6 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.

7 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu.

8 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka na mje katika nyua zake.

9 Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake; dunia yote na itetemeke mbele zake.

10 Semeni katika mataifa kwamba, “Mwenyezi Mungu anatawala.” Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; atawahukumu watu kwa uadilifu.

11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake;

12 mashamba na yashangilie, pamoja na vyote vilivyomo. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;

13 itaimba mbele za Mwenyezi Mungu kwa maana anakuja, anakuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa katika kweli yake.