Zaburi 113

1 Msifuni Mwenyezi Mungu. Enyi watumishi wa Mwenyezi Mungu msifuni, lisifuni jina la Mwenyezi Mungu.

2 Jina la Mwenyezi Mungu na lisifiwe, sasa na hata milele.

3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake, jina la Mwenyezi Mungu linapaswa kusifiwa.

4 Mwenyezi Mungu ametukuka juu ya mataifa yote, utukufu wake juu ya mbingu.

5 Ni nani aliye kama Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, Yule aliyeketi kwenye kiti cha enzi huko juu,

6 ambaye huinama atazame chini aone mbingu na nchi?

7 Huwainua maskini kutoka mavumbini, na kuwanyanyua wahitaji kutoka lundo la majivu,

8 huwaketisha pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake.

9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, akiwa mama watoto mwenye furaha. Msifuni Mwenyezi Mungu.