Zaburi 11
1 Kwa Mwenyezi Mungu ninakimbilia. Unawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege utorokee kwenye mlima wako.
2 Hebu tazama, waovu wanapinda nyuta zao; wanaweka mishale kwenye nyuzi zake ili wakiwa gizani, wawapige walio wanyofu wa moyo.
3 Wakati misingi imeharibiwa, mwenye haki anaweza kufanya nini?”
4 Mwenyezi Mungu yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; Mwenyezi Mungu yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawachunguza.
5 Mwenyezi Mungu huwachunguza wenye haki, lakini nafsi yake inachukia waovu na wale wanaopenda mapigano.
6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka; upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
7 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, yeye hupenda haki. Wanyofu watauona uso wake.